Breaking News
recent

Kwanini hayati Abeid Aman Karume alipiga marufuku ndondi visiwani Zanzibar?

Ndondi Zanzibar
Mchezo wa Masubwi (ndondi) ni moja kati ya michezo mikubwa na yenye umaarufu mkubwa dunia kote, lakini mchezo huu ni marufuku kuchezwa katika visiwani Zanzibar.
Je ni kwanini? mchezo huu haurusiwi kuchezwa katika visiwa hivyo vya Marashi ya karafuu.
Jibu la Swali hili ni la kihistoria, katazo la kutopigana kwa vijana wa kizanzibar lilitolewa na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume, baada ya visiwa hivyo kujitawala baada ya mapinduzi wa mwaka 1964.
Abeid Aman Karume, ndie aliyetoa kauli ya kukataza kuchezwa ngumi baada ya kualikwa kwenye pambano la masumbwi ambalo liliandaliwa na raia mmoja wa Ghana.
Alipofika katika eneo hilo ndipo mzee Karume alipotoa kauli ya marufuku kuchezwa masumbwi.
"Alipofika pale aliangalia na kuuliza kwanini wanataka kupigana. Alipoambiwa ni mchezo wa ndondi akasema mwisho leo, kwa vijana wa Kizanzibar - 'kupigana masumbwi ni kufanywa kama watumwa'" anaeleza waziri wa vijana, utamaduni, sanaa na michezo visiwani Zanzibar, Balozi Ally Abeid Karume, ambae pia ni mtoto wa Marehemu Karume.
Balozi Ally Karume, anaeleza zaidi kuwa hayati Karume alifikia uamuzi pia kwa kuzingatia historia ya namna Visiwa vya Zanzibar vilivyopata Uhuru wake kwa mapinduzi, hivyo kuhusisha kupigana huko kuwa sawa na kuendelea kuwa chini ya wakoloni.
Ndondi Zanzibar
"Katika sera ya michezo mzee Karume alisema tufanye michezo ambayo ni mizuri na yenye maadili, michezo yoyote yenye madhara na sisi na madhara yanayoonekana na yasiyooneka, michezo hiyo tusiicheze na tuipige marufuku".
Maamuzi haya ya miaka mingi ni sukari chungu kwa mabondia wengi walioko Visiwani Zanzibar, mabondia wanaruhusiwa kufanya mazoezi tu lakini kupigana ni aidha wapigane Tanzania bara au nje ya nchi.
Hasani Bandani ni bondia ambae amepigana mapambano manne nje ya Zanzibar, lakini anaishi na kufanya mazoezi yake katika katika eneo la Welezo Tai Boxing bandani Visiwani.
Anasema, "Kitu kinachoturejesha nyuma hapa kwetu ni kutocheza ili hali tunafanya mazoezi kila siku na hatuwezi kupigana mpaka tutoke nje ''.
Katika eneo anakofanyia mazoezi Hassani Bandani, kuna zaidi ya mabondia kumi wa uzani tofauti wanaofanya mazoezi ya Karate, ndondi, na mchezo wa Makonde na Mateke (kickboxer) na kilio chao kikubwa ni kwa Serikali ya mapinduzi Zanzibar kuwaruhusu kucheza mchezo wanaoupenda katika ardhi yao ya nyumbani.
Ndondi Zanzibar
Licha ya mabondia waliopo kutocheza katika mapambano yoyote visiwani humo, bado wanakumbwa na changamoto ya kukosa vifaa kwa kuwa vifaa vya michezo huwa ni ghali na hawana uwezo wa kujimudu kununua.
Pamoja na mabondia na wachezaji wa michezo ya mapigano kuiomba Serikali ya mapinduzi kuwapa ruksa ya kuanza kucheza mchezo wa ngumi wakiwa nyumbani kwao, Serikali kupitia kwa Waziri wa Michezo, Balozi Ally Abeid Karume, amesisitiza kuwa katazo la mchezo huo litaendelea kama lilivyoelekeza na Hayati Abeid Aman Karume.
"Nimebahatika kuwa waziri wa wizara ya michezo basi nitilie mkazo kwenye hili, haturudi nyuma hapa Zanzibar hapana rukhsa kupigana ngumi ila wakitaka wakapigane Tanzania bara na kwingine duniani na tunawaomba washinde ila wasiue mtu''.
Sport Nyumbani

Sport Nyumbani

No comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.