Breaking News
recent

Hizi hapa dili zilizokwama dakika za majeruhi kiangazi EPL 2019-10

Leroy Sane (City-Bayern) 
Kwa kipindi kirefu cha usajili wa majira ya kiangazi, jina la Sane lilikuwa likihusishwa na Bayern Munich, hata kufikia hatua ya kocha wa timu hiyo ya Bundesliga, Niko Kovac, kuomba radhi kwa kauli yake kwamba walikaribia kumnasa.
Hadi zikiwa zimebaki saa chache kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili usiku wa kuamkia jana, Sane alikuwa akiwindwa na Bayern, ikielezwa kuwa tayari mabingwa hao wa Bundesliga waliweka mezani kiasi cha Pauni milioni 140.
Paulo Dybala (Juve-Tottenham) 
Alitajwa kuwa njiani kwenda Tottenham, lakini hadi dirisha la usajili linafungwa, hakuna kilichotokea.
Hata hivyo, haikuwa Tottenham pekee, pia Manchester United nayo ilikuwa ikiinyemelea saini ya Paulo Dybala. Lakini sasa, hadi dirisha la usajili linafungwa, nyota huyo wa kimataifa wa Argentina alibaki  Juve, wababe wa Serie A.
Kurt Zouma (Chelsea-Everton)
Zouma alikuwa silaha ya safu ya ulinzi ya Everton msimu uliopita akicheza kwa mkopo akitokea Chelsea. Hivyo, Everton wao walitaka kumbakiza kwa matumizi ya msimu ujao, jambo lililoshindikana hadi kufungwa kwa usajili usiku wa kuamkia jana.
Hata katika mitandao ya kijamii, wakati mashabiki wa Chelsea wakitaka abaki, wale wa Everton walikuwa wakishinikiza abaki katika eneo la beki wa kati msimu ujao.
Wilfried Zaha (C. Palace-Everton)
Hiyo ni filamu nyingine ya usajili wa kipindi ya kingazi. Tayari Zaha alishawaambia mabosi wake wa Palace kwamba anataka ‘kusepa’ zake. Hadi kufikia dakika za mwisho kabla ya kufungwa kwa usajili ni Everton ndiyo iliyokuwa imebaki kumfukuzia winga huyo.
Hata hivyo, huenda kilichokwamisha dili hilo ni dau walilokuwa wakilitaka Palace, yaani Pauni milioni 80.
Dayot Upamecano (RB Leipzig-Arsenal)
Baada ya safu yake ya ulinzi kupitisha mabao 51 ya Ligi Kuu msimu uliopita, kocha wa Arsenal, Unai Emery, alitaka kuipa makali.
Baada ya nahodha wake, Laurent Koscielny, kuhamia Bordeaux, Emery alimtolea macho beki wa RB Leipzig, Dayot Upamecano. Dili lilishindikana baada ya Leipzig kusisitiza kuwa wanataka Pauni milioni 70.
Christian Eriksen (Tottenham-Man United)
Hatima ya kiungo Christian Eriksen pale Tottenham imekuwa shakani tangu kufunguliwa kwa dirisha la usajili. Hapo ndipo klabu ya Real Madrid ilipojisogeza, kabla ya Manchester United ‘kuuteka’ mpango huo.
Tayari Man United walishatajwa kuwa kwenye mazungumzo na kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino, juu ya dili hilo, ikielezwa kwamba jana nyota huyo wa kimataifa wa Denmark angeelekea zake Old Trafford.
Dili lilivurugika kwa kile kilichoelezwa kwamba Eriksen ameonesha nia ya kwenda Hispania, kwa maana ya kujiunga na Madrid.
Paul Pogba (Ma United-Madrid)
Kukwama kwa dili hilo kumetajwa kumchefua kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane, ambaye ameelezwa kumnunia raia wa klabu hiyo, Florentino Perez.
Zidane alidhani angeipata saini ya Mfaransa mwenzake huyo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili la kiangazi, asijue Pogba atabaki Old Trafford.
Madrid wameshindwa kuinasa saini ya Pogba, licha ya kwamba tayari alishaelezwa kutokuwa na uhusiano mzuri na kocha wake, Ole Gunnar Solskjaer, ikifikia hatua ya mkufunzi huyo raia wa Norway kutaka apigwe bei tu.
Sasa, baada ya kukwama kwa mpango wao usiku wa kuamkia jana, zipo taarifa zinazodai kwamba Madrid wameamua kuigeukia saini ya Neymar ifikapo Januari, mwakani, wakati wa usajili wa dirisha dogo (majira ya baridi).
5 Bora dili za bei kali
* Harry Maguire (Leicester-Man United): Pauni mil 80 (Sh bil. 222 za Tanzania)
*Nicolas Pepe (Lille-Arsenal): Pauni mil 72 (Sh bil. 200)
*Rodri (Atletico-Man City): Pauni mil 63 (Sh bil. 175)
 *Joao Cancelo (Juve-Man City): Pauni mil 60 (Sh bil. 167)
*Tanguy Ndombele (Lyon-Tottenham): Pauni mil 54 (Sh bil. 150)
Dili zilizotiki ‘jioni’ 
 *Danny Drinkwater (Chelsea-Burnley)
*Giovani Lo Celso (Real Betis- Tottenham)
*Andy Carroll (West Ham-Newcastle)
*Kieran Tierney (Celtic-Arsenal)
*Romelu Lukaku (Inter- Man United) 
Sport Nyumbani

Sport Nyumbani

No comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.