Breaking News
recent

Bifu lamuondoa David Luiz Chelsea

LONDON, England
SABABU ya beki Mbrazili, David Luiz, kuitaka Arsenal muda mfupi baada ya kutoonekana mazoezini na wenzake Chelsea wiki hii, imetajwa kuwa ni bifu lililopo kati yake na kocha, Frank Lampard.
Arsenal ndio iliyokuwa klabu ya mwisho kuhusishwa na beki huyo hadi kufikia jana ambayo ndio ilikuwa siku ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi kwa Ligi Kuu England.
Ripoti zilizoanza kuibuka tangu juzi, Jumatano, zilieleza kuwa Luiz hakuonekana katika mazoezi na wenzake Chelsea, chini ya kocha wao mpya, Lampard, na aliitaka klabu hiyo imruhusu ahamie Arsenal.
Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Mirror, ni kwamba Luiz hana mahusiano mazuri na Lampard tangu walivyokuwa wanacheza wote Stamford Bridge, kabla ya Lampard kustaafu na kurejea tena akiwa kocha.
Hakuna aliyetegemea kuona Luiz, 32, akiondoka Chelsea mwezi huu na kuelekea Arsenal kwa kitita cha pauni milioni 8, kwani ilionekana wazi kuwa atauanza msimu huu akiwa darajani.
Kwa mujibu wa mtandao wa The Telegraph, ni kwamba Lampard alimwondoa Luiz kwenye mazoezi na wenzake, kabla ligi kuu haijaanza kutimua vumbi leo, hasa baada ya beki huyo kuanza ‘utata’.
Ilielezwa kuwa, Lampard alimtaka Luiz afanye mazoezi mbali na wenzake wa kikosi cha kwanza kuelekea mchezo wao wa kwanza msimu huu dhidi ya Man United kabla ya kutua Arsenal jana.
Historia inaonesha kuwa Luiz na Lampard waliwahi kurushiana maneno mwaka 2013, katika mchezo wa Ligi ya Europa ambao Chelsea walibamizwa mabao 3-2 na Rubin Kazan.
Katika mechi hiyo, Lampard alionekana kumshukia mchezaji mwenzake (Luiz), juu ya majukumu yake ya ulinzi, ‘akidonoa’ kidole chake kwenye kifua cha beki huyo na kujibizana wakati wakielekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Mtifuano huo uliamuliwa na mchezaji wa zamani wa Chelsea, Yossi Benayoun, ambaye aliamua kuchukua jukumu la kuwapatanisha na baadaye, kocha wao, Rafa Benitez alizungumzia tukio hilo mbele ya waandishi wa habari.
“Unapoona wachezaji wako wanajibizana kuhusu vitu vinavyotokea uwanjani ujue ni jambo zuri, hapo ndio mwanzo wa kupata suluhisho wakati wa mapumziko. Ni jambo la kawaida,” alisema Benitez.
Baada ya msimu wa pili akiwa Chelsea, Luiz alitimkia PSG kwa kitita cha pauni milioni 50, huku Lampard naye akiondoka mwaka 2014. Luiz alirejea Chelsea baada ya miaka miwili na kufanikiwa kunyakua EPL akiwa chini ya kocha, Antonio Conte, lakini hakutaka kubaki tena hapo licha ya kusisitiza kwamba alikuwa na furaha.
Sport Nyumbani

Sport Nyumbani

No comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.