Mlinzi wa kati wa klabu ya Paris St Germain ya Ufaransa ambaye ni raia wa Brazil, MARQUINHOS amevunja rekodi ya Gwiji wa Liberia, George Weah iliyodumu kwa miaka 21 katika klabu ya Paris Saint Germain.
Marquinhos mwenye miaka 20 amefikisha mechi 34 mfululizo akiwa uwanjani bila nyavu za timu hiyo kuguswa kufuatia ushindi wa mabao 4-0 waliopata kwenye mechi ya ligi kuu nchini humo dhidi ya Bastia mwishoni wa juma lililopita.
Weah aliweka rekodi ya kucheza mechi 33 tangu msimu 1993-94 katika timu hiyo yenye maskani yake mji mkuu wa Ufaransa bila kufungwa goli.
Kwa mujibu wa Maofisa wa PSG, hakuna mchezaji yeyote ambaye amewahi kukaribia rekodi hiyo tangu kuanzishwa kwa timu hiyo miaka 44 iliyopita.
Marquinhos alijiunga na PSG kutoka Roma ya Italia mwaka 2013 na amecheza mechi 40 akiwa na kikosi cha mabingwa hao wa Ufaransa akifunga magoli manne.
Weah aliyekuwa mshambuliaji , alijiunga na PSG akitokea Monaco mwaka 1992 na alikaa misimu mitatu katika dimba la Parc des Princes akifunga magoli 32 katika mechi 96 alizocheza.
Alishinda tuzo ya FIFA ya mchezaji bora wa dunia mwaka 1995 na ndiye Muafrika pekee aliyeshinda tuzo hiyo ya heshima.
No comments:
Post a Comment