Breaking News
recent

Twiga Stars sasa Fit kuivaa Zambia, Wakabidhiwa Bendera ya Taifa leo

DSC07412-e1426768168708Nahodha wa timu ya Taifa ya wanawake Sofia Edward Mwasikili (kushoto) akikabidhiwa bendera ya Taifa na katibu mkuu wa TFF Selestine Mwesigwa (kulia) katikati ni kocha wa timu hiyo Rogasian Kaijage.
Timu ya Taifa ya soka la wanawake (Twiga Stars) leo imeagwa kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF Karume jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuondoka kuelekea Zambia kucheza mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa upande wa soka la wanawake.
Akiwakabidhi bendera ya Taifa katibu mkuu wa TFF Selestine Mwesigwa amesema, Twiga Stars inakwenda kuliwalisha Taifa lakini pia wanapata nafasi ya kuonekana kimataifa ili kuonesha vipaji vyao.
“Niwaambie tu wachezaji, hapa mnakwenda kuwakilisha Taifa la Tanzania na pia mnapata nafasi ya kuonekana kimataifa, mpira wa wanawake sikuhizi umekua na tumekua tukipokea barua mara kwa mara kutoka kwa mawakala wakiulizia kama wanaweza kupata wachezaji wakike kwa ajili ya timu za huko Ulaya,” amesema Mwesigwa.
“Tunakwenda kucheza na Zambia, mwaka jana tulicheza nao lakini mambo hayakuwa mazuri kwasababu tulitoka nao sare hapa tukapoteza mechi kwao na tukawa tumeondolewa kwenye mashindano. Lakini kwa mujibu wa mwalimu na benchi zima la ufundi wamesema safari hii lazima tuwaondoe Zambia,” aliongeza Mwesigwa.
Kwa upande wa kocha wa timu hiyo Rogasian Kaijage yeye amesema kuwa, anakiamini kikosi chake na wanakwenda kushindana na watashinda kwa sababu mwaka huu wamejiandaa vizuri ukilinganisha na mwaka jana.
“Nina uhakika na kikosi changu na tunakwenda Zambia kupambana ili turudi na ushindi, mwaka huu tumejiandaa vizuri ukilinganisha na mwaka jana. Tunaomba watanzania watuunge mkono, watuombee na kwa hali waliyonayo vijana basi lazima tutarudi na ushindi,” Kaijage alisema.
Naye nahodha wa Twiga Stars Sofia Edward Mwasikili amesisitiza kuwa kwa maandalizi waliyoyafanya ni lazima warejee nyuambani na ushindi.
“Kwanza nawashukuru viongozi kwa kuja kutuaga, pili nawaahidi tutarudi nyumbani na ushindi kwa sababu tumefanya maandalizi ya kutosha na tunakwenda Zambia kushindana na siyo kushiriki” Sofia alisisitiza.
Msafara wa watu 25 wakiwemo wachezaji 18 na viongozi saba unatarajiwa kuondoka saa tisa usiku na ndege ya shirika la Ethiopia kuelekea Zambia, Twiga Stars itacheza mechi yake siku ya Jumapili, kama Twiga Stars watafanikiwa kuitoa Zambia watakuwa wamekata tiketi ya kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika kwa upande wa soka la wanawake.
Sport Nyumbani

Sport Nyumbani

No comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.