
KUNA watu bado wanazi sana. Mmojawapo ni mkimbiaji aliyeiteka dunia katika mbio fupi, Usain Bolt wa Jamaica ambaye anajulikana kwa mapenzi yake kwa mabingwa wa zamani wa England, Manchester United.
Bolt ameionya Kampuni ya Puma ambayo inamdhamini, kuachana na wazo la kumvalisha jezi ya klabu ya Arsenal ambayo pia inadhaminiwa na kampuni hiyo, kwa madai kwamba hawezi kuvaa jezi ya adui.
Bingwa huyo wa dunia wa mbio za mita 100 na 200 amekuwa akidhaminiwa na Puma tangu mwaka 2003, huku Arsenal ikiwa imeanza kuvaa jezi za Puma katika msimu huu huku wakilipwa dau la Pauni 30 milioni kwa mwaka katika mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Pauni 150 milioni.
Hata hivyo, licha ya mapenzi yake kwa Kampuni ya Puma, Bolt amedai kwamba hakuna kiasi chochote cha pesa ambacho kinaweza kumfanya aisaliti timu yake ya Manchester United kwa kuvaa jezi ya Arsenal japo kwa tangazo la biashara tu.
“Nimewaambia Puma sitapiga picha zozote nikiwa nimevaa jezi za Arsenal. Nimewaambia sitaki hata waniombe,” alisema Bolt hivi karibuni.
Mkiambiaji huyo ambaye ametangaza kustaafu mbio kuanzia mwaka 2017 baada ya michuano ya dunia, ameeleza vile vile jinsi asivyoielewa staili ya soka ya kocha wao wa sasa hivi, Louis van Gaal.
“Kwangu mimi kama unaanzisha staili mpya nadhani kwanza inabidi uifanyie kazi kama timu inaweza kumudu. Sidhani kama njia zake za upigaji pasi anazotaka zitaweza kufanya kazi Manchester United. Labda kama akibadili wachezaji wote,” alisema Bolt.
“Najaribu kuzitazama timu kwa soka la kupasiana, lakini man United siyo timu ya namna hiyo. Kama tungekuwa na Giggs na Scholes pale katikati, ingeweza kuwa vizuri.
Mata ni mzuri lakini ni mfupi sana. Rooney ni mzuri lakini anacheza taratibu na kiungo inabidi uwe na kasi. Kama ilivyo kwa Hazard au baadhi ya wachezaji wa Arsenal,” aliongeza Bolt.
Bolt anaamini kama angeamua kuwa mwanasoka, mchezo ambao anaupenda sana, angependa kucheza kama winga wa upande wa kushoto na kukimbiza mabeki wa timu pinzani kwa kasi kubwa.
No comments:
Post a Comment