Breaking News
recent

Tambwe aiduwaza CAF

Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akifunga goli kwa kichwa dhidi ya BDF IX ya Botswana  



MSHAMBULIAJI wa Yanga, Amissi Tambwe amefanikiwa kucheza mechi ya kwanza ya mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ndani ya ardhi ya Tanzania.
Katika hilo Tambwe pia amefanikiwa kuweka rekodi moja ya awali katika soka la Afrika, rekodi ambayo itaendelea kuwa katika kumbukumbu za CAF.
Yanga ambayo inashiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, wikiendi iliyopita ilivuna ushindi wa kwanza wa mabao 2-0 dhidi ya BDF XI ya Botswana yote yakifungwa na Tambwe.
Katika mechi 23 za Kombe la Shirikisho zilizochezwa katika siku mbili za Februari 14 na 15, jumla ya mabao 43 yalifungwa katika mechi hizo lakini mabao mawili pekee ndiyo yameweka rekodi ya kufungwa mapema zaidi yakifungwa na timu mbili kutoka Afrika Mashariki.
Rekodi ambayo Tambwe amefanikiwa kuiweka Afrika ni juu ya bao la mapema ambapo mpaka mechi za kombe hili zikikamilika jana alikuwa yeye na kiungo mwingine wa Afrika Mashariki wakifunga mabao hayo ya mapema.
Tambwe aliifungia Yanga bao dakika ya kwanza ya mchezo huo dhidi ya BDF XI kwa kichwa akipokea krosi ya kiungo Haruna Niyonzima.
Mbali na Tambwe kiungo wa Rayon Sport ya Rwanda Leon Uwambazimana amefanikiwa kufungana na Tambwe baada ya kufanikiwa kuifungia timu hiyo yenye mashabiki wengi Rwanda bao hilo pekee katika dakika ya kwanza wakati walipoumana na Panthere ya Cameroon.
Achana na hilo, Tambwe, mshambuliaji mtulivu kutoka Burundi aliyevuna Dola 20,000 (Sh34 milioni) katika usajili wake akitokea Simba, mpaka sasa amefanikiwa kuweka rekodi nyingine katika kikosi cha Yanga baada ya kuzifunga timu mbili tofauti mabao manne yote akitumia kichwa.
Ipo hivi; Tambwe mpaka anaondoka Simba katika nusu ya mzunguko wa kwanza alifanikiwa kuifungia timu hiyo bao moja pekee dhidi ya Coastal Union akitumia krosi ya Emmanuel Okwi wakati timu hizo zikitoka sare ya mabao 1-1.
Akiwa Yanga Tambwe amefanikiwa kufunga mabao matatu moja akifunga dhidi ya Azam katika Ligi Kuu Bara ukiwa mchezo wake wa kwanza tangu asajiliwe akifunga kwa kichwa akitumia krosi ya kiungo mkabaji, Salum Telela.


Kama haitoshi Februari 14 Jumamosi iliyopita alifungua ukurasa wake wa mabao ya Kimataifa ndani ya timu hiyo akiyafunga kwa kichwa akitumia krosi za Niyonzima na winga Mrisho Ngassa na hivyo kulitangaza jina lake Afrika kwa rekodi hiyo.
Sport Nyumbani

Sport Nyumbani

No comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.